Dk Slaa  akiwa  na  mke   wake  siku  alipofanya   ziara  marekani




Makala Dk Willibrod Peter Slaa: Muadilifu na mchapa kazi mwenye nakisi ya hekima na weledi
Kitila MkumboToleo la 377 29 Oct 2014 DK. Wilbrod Peter Slaa ni mwanasiasa pekee wa upinzani aliyedumu na mvuto wa kisiasa kwa muda mrefu zaidi kuliko mwanasiasa mwingine yeyote wa upinzani nchini Tanzania. Katika siku za hivi karibuni ametajwa kuwa ndiye mgombea wa urais kinara wa kambi ya upinzani kupitia kundi la UKAWA. Katika makala haya tunajadili wasifu wa mwanasiasa huyu katika maeneo ya uadilifu, uchapa kazi, hekima na weledi. Dk. Slaa alizaliwa Oktoba 29, 1948 katika Kijiji cha Kwermusl, Wilayani Mbulu. Alisoma Shule ya Msingi Kwermusl mwaka 1958-1961 na Shule ya Kati (Middle School) ya Karatu 1962-1965. Baada ya kufaulu mtihani wa Darasa la Nne, Dk. Slaa hakuendelea na masomo katika shule za serikali bali alijiunga na Seminari ya Dung’unyi Mkoani Singida mwaka 1966-1969 kwa masomo ya sekondari. Alifaulu mtihani wa Kidato cha Nne vizuri na kuchaguliwa kujiunga na Kidato cha tano katika Seminari ya Itaga Mkoani Tabora alikosoma kati ya mwaka 1970 na 1971. Ni katika seminari za Dung’unyi na Itaga ambapo Dk. Slaa alifanya uamuzi kamili wa kuwa mtumishi wa Kanisa Katoliki. Alipomaliza Kidato cha Sita katika Seminari ya Itaga alijiunga na Seminari ya Kibosho kwa muda wa mwaka mmoja yaani 1972-1973 na kutunukiwa Stashahda ya Falsafa ambayo ilimwezesha kujiunga na Seminari Kuu ya Kipalapala mkoani Tabora akisomea zaidi falsafa na theolojia kati ya mwaka 1974 na 1977. Hii ni kati ya seminari kuu za Kanisa Katoliki nchini ambazo huandaa mapdri, sambamba na seminari za Segerea na Peramiho. Ni katika Seminari Kuu ya Kipalapala ambako Dk. Slaa alianza kuonyesha alama ya uongozi ambapo alichaguliwa kuwa Rais wa Wanafunzi katika seminari hiyo. Katika kipindi alipokuwa Seminari ya Kipalapala Dk. Slaa alisoma pia Diploma ya Theolojia katika Chuo Kikuu cha Makerere nchini Uganda. Alipata upadirisho kamili mwaka 1977. Baada ya kutumikia upadri kwa miaka miwili alijiunga na Chuo Kikuu cha Pontifical Urbaniana nchini Italia akisomea udaktari wa Sheria za Kanisa maarufu kama J.C.D. (Juris Canonici Doctor ) au I.C.D. (Iuris Canonici Doctor) kati ya mwaka 1979 na 1981. Kwa mfumo wa Kanisa Katoliki, hii ndiyo shahada ya juu kabisa katika masomo ya sheria ya kanisa. Kwa mlolongo wa elimu yake tunaweza kusema kwamba Dk. Slaa ni kati ya wanasiasa waliosoma vizuri nchini Tanzania, pamoja na kwamba hakupitia katika mfumo wa kawaida wa elimu unaotambulika Tanzania. Kwa mfumo wetu wa elimu, mtu huhitajika kuwa na shahada ya umahiri kabla hajaruhusiwa kujiunga na masomo ya shahada ya uzamivu. Sifa moja ya kitaaluma aliyo nayo Dk. Slaa ni uwezo wa kuandika. Amewahi kuandika vitabu viwili ambavyo ni “Utimilifu wa Msichana” na “Utimilifu wa Mvulana”. Hii ni sifa nadra kwa viongozi wetu wengi. Ukiacha upadri, Dk. Slaa alifanya kazi mbalimbali katika taasisi za Kanisa Katoliki nchini Tanzania. Aliwahi kuwa Msaidizi wa Askofu na Mkurugenzi wa Maendeleo katika Jimbo la Mbulu. Mwaka 1986, alichaguliwa kuwa Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC). Hiki ni chombo cha juu kabisa kinachosimamia shughuli zote za Kanisa Katoliki nchini Tanzania. Alidumu katika nafasi ya Katibu Mkuu wa TEC kwa muda wa miaka tisa akiwa ametumikia mihula yote mitatu. Kwa mujibu wa taarifa rasmi ndani ya Kanisa Katoliki na watu waliofanya naye kazi kwa karibu, Dk. Slaa anaelezwa kwamba ndiye Katibu Mkuu mwenye ufanisi zaidi tangu TEC ianzishwe. Miundo mbinu mingi tunayoiona ya Kanisa Katoliki nchini ilianzishwa na kukamilishwa katika kipindi ambacho Dk. Slaa alikuwa Katibu Mkuu wa TEC. Nilipozungumza na mmoja wa viongozi wa Kanisa Katoliki anayeheshimika sana hapa nchini alinieleza kwamba sifa kubwa ya Dk. Slaa alipokuwa TEC ni uchapa kazi na uadilifu wa hali ya juu. Hizi ni sifa ambazo mimi binafsi naweza kuzishuhudia baada ya kufanya naye kazi ndani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA). Dk. Slaa aliacha upadri muda mfupi baada ya kumaliza muhula wake kama Katibu Mkuu wa TEC. Wengi wetu hatuelewi mazingira ya Dk. Slaa kuacha upadri na kuna baadhi ya mahasimu wake kisiasa wamekuwa wakitumia hili kama silaha kisiasa wakienda mbali hata kutuhumu kwamba alifukuzwa kwa sababu za kimaadili. Ukweli ni kwamba Dk. Slaa aliacha upadri kwa kufuata taratibu kamili ndani ya Kanisa Katoliki na aliacha yeye mwenyewe bila kushinikizwa, kufukuzwa au hata kupewa onyo. Kwa maelezo yake ni kwamba kuna mambo ambayo aliyakataa ndani ya Kanisa na kwa dhamira yake asingeweza kuendelea. Amepata kukaririwa akisema kuwa mambo hayo ni binafsi na asingependa kuyaeleza zaidi. Kisiasa, tunaweza kusema Dk. Slaa ni zao la ujinga na ubabe wa viongozi ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM). Aliingia rasmi katika siasa za kitaifa mwaka 1995 alipogombea ubunge kupitia CCM na kushinda kura za maoni lakini jina lake liliondolewa kwa kile ambacho yeye anakieleza kwamba “jina liliondolewa kimizengwe kwa msingi kwamba hakuwa mwenzao”. Baada ya kunyang’anywa ushindi wake katika kura za maoni, Dk. Slaa aligombea kupitia CHADEMA na kushinda. Alikuwa Mbunge wa Karatu kwa vipindi vitatu mfufulizo kutoka mwaka 1995 hadi mwaka 2010 alipogombea urais. Ndani ya CHADEMA alipata kuwa Makamu Mwenyekiti mwaka 1998 hadi mwaka 2004 na amekuwa Katibu Mkuu kutoka 2004 hadi sasa. Kifamilia, Dk. Slaa alipata kumuoa mbunge machachari wa Viti Maalumu CHADEMA, Rose Kamili na kuzaa naye watoto wawili, Emiliana Slaa na Linus Slaa. Waliachana na Rose muda mfupi kabla ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010. Sasa anaishi na Josephine Mushumbushi na wamezaa naye mtoto mmoja maarufu kwa jina la Junior. Josephine ni mwana mama mwingine machachari anayefananishwa kihaiba na Lucy Kibaki, aliyekuwa First Lady wa Kenya. Maeneo matatu ni muhimu katika kutathmini nafasi ya Dk. Slaa katika mbio za urais. Maeneo haya ni uchapa kazi, uadilifu na hekima. Watu waliofanya naye kazi sehemu mbalimbali na hasa ndani ya Kanisa Katoliki wanakiri kwamba moja ya sifa kubwa ya Dk. Slaa ni uchapa kazi. Katika hili mimi mwenyewe ni shuhuda pale nilipofanya naye kazi ndani ya CHADEMA. Dk. Slaa ana sifa moja adhimu kwa wanasiasa walio wengi nchini mwetu, nayo ni kujali muda. Katika mikutano yote niliyopata kuhudhuria na Dk. Slaa sikumbuki ni lini alichelewa. Mara zote hufika katika chumba cha mkutano mapema hata kabla ya wasaidizi wake na atakaa muda wote akisubiri wajumbe wengine bila kujali nafasi yake. Hii ni sifa inayomtenga kwa mbali na wanasiasa wengi ndani na nje ya chama chake. Wanasiasa wetu wengi hawajali muda na huenda kwenye matukio muhimu kwa kuchelewa mno na hawajali kabisa kuchelewa kwao. Moja ya dalili muhimu ya uchapa kazi ni kujali muda. Aidha, anapokuwa kwenye shughuli za chama chake, Dk. Slaa hakuna kitu kitakachomtoa nje. Ukiwa naye katika msafara hakikisha umekula kabisa kwa sababu yeye mwenyewe hajali kushinda njaa hata siku nzima madamu kazi aliyoenda kuifanya haijasha. Hali hii pia imeshuhudiwa na baadhi ya wakurugenzi wa Halmashauri za Wilaya pamoja na wajumbe wenzake waliofanya naye kazi alipokuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Serikali za Mitaa. Eneo la pili ni uadilifu. Hakuna shaka kwamba Dk. Slaa ni muadilifu. Hakuna popote alipofanya kazi utakapokutana na harufu ya shutuma yeyote kuhusu yeye kudokoa mali ya umma au kutumia madaraka yake kwa njia ya kujinufaisha. Hii ni ndani ya Kanisa Katoliki, Bungeni na hata katika chama chake. Hiyo nayo ni sifa nadra miongoni mwa wanasiasa wetu. Hata hivyo, Dk. Slaa haonyeshi kama mtu anayeweza kudhibiti ufisadi. Tunamuona zaidi katika taswira hii kwa kuangalia utendaji wake ndani ya CHADEMA kama Katibu Mkuu. Kumekuwa na malalamiko ya muda mrefu ndani ya chama chake kuhusu matumizi mabaya ya mali za chama hicho. Kwa mfano, mara nyingi Mwenyekiti wa sasa wa CHADEMA ametuhumiwa kukikopesha chama bila utaratibu wala kumbukumbu yoyote ya nyaraka na kisha kudai chama kimlipe. Pale palipohojiwa inakuwaje chama kilipe deni ambalo hatujui lilikopeshwaje Dk. Slaa amekuwa mtu wa kwanza katika kumtetea. Aidha Mwenyekiti ameshutumiwa mara nyingi kwamba amekuwa ndiye mnunuzi wa vifaa vya chama nje ya nchi pasipokufuata utaratibu wowote wa kitenda kama ilivyo kwenye katiba na sheria za nchi. Bahati nzuri madai haya yamethibitishwa na ripoti ya CAG iliyoonyesha kwamba ununuzi ya magari ya chama hicho ulifanyika bila kufuata utaratibu wa kitenda na hivyo kusababisha chama hicho kupata hati ya kutia shaka. Kutofuata utaratibu kunakoelezwa katika Ripoti ya CAG ni kati ya matendo ambayo Dk. Slaa amekuwa akiyapigia kelele katika serikali lakini ambayo ameshindwa kuyadhibiti ndani ya chama chake. Matokeo yake ndiyo hayo kwamba chama chake kinapata hati ya shaka katika kipindi ambacho kilipaswa kuonyesha mfano na utofauti na CCM. Kwa hivyo, katika eneo la uadilifu tunamuona Dk. Slaa kama mpiga mbinja (whistle blower) wa kuwazomea mafisadi lakini si mtu anayeweza kudhibiti ufisadi. Eneo la pili ni hekima na weledi. Kwa kiasi fulani Dk. Slaa ameonyesha weledi katika utendaji wake wa kazi. Kwa mfano, wakati tunaandika ilani ya CHADEMA kwa ajili ya uchaguzi wa mwaka 2010, Dk. Slaa ni miongoni mwa viongozi watatu pekee, sambamba na Profesa Mwesiga Baregu na Zitto Kabwe, ambao waliweza kusoma na kutoa maoni yao katika ilani hiyo. Kilichonishangaza zaidi ni wepesi wa Dk. Slaa kusoma na kurudisha maoni yake mapema iwezekanavyo na hata kupiga simu na kufafanua alichokuwa anamaanisha katika maoni yake. Aidha, alipokuwa katika mizunguko ya kampeni zake alipofika Dodoma Vijijini alikutana na nyumba duni sana za wananchi ambazo ilionekana alikuwa hajaziona maishani mwake. Mara moja alinipigia simu kama mtu niliyekuwa naratibu ilani ya chama na kuniagiza niingize swala la kuboresha makazi katika ilani. Hivi ndivyo sera ya CHADEMA kuhusu makazi ilivyozaliwa na kuweka bayana kwamba kodi ya vifaa vya ujenzi ingeshushwa chini ya utawala wa CHADEMA ili kuwapa wananchi unafuu wa kununua vifaa hivyo kwa bei rahisi. Hata hivyo, kuna maeneo kadhaa ambayo yanatia shaka kuhusu hekima na hata weledi wa Dk. Slaa. Nitatoa mifano michache. Mfano mmoja ni wakati wa kampeni za mwaka 2010 pale alipoibuka na madai kwamba lori moja huko Tunduma lilikuwa limekamatwa likiwa limesheheni masanduku ya kupiga kura. Kipindi kifupi baadaye akaibuka na madai mengine kwamba mgombea wa CCM, Rais Jakaya Kikwete alikuwa ameonekana katika Hoteli ya Lakairo Jijini Mwanza wakiwa wanapanga mikakati ya kuiba kura. Madai yote yalikuja kuthibitika kwamba hayakuwa na chembe hata ndogo ya ukweli. Mfano wa pili ni msimamo wa Dk. Slaa kuhusu mahusiano ya Tanzania na Rwanda. Wakati majeshi ya nchi yetu yakiwa nchini Kongo yakipigana na waasi wa M23 alitoa kauli ya kukosoa msimamo wa Tanzania kupeleka majeshi yetu katika nchi hiyo na kuonekana kuunga mkono msimamo wa Rais Paul Kagame, jambo ambalo lilishangiliwa sana na vyombo vya habari nchini Rwanda. Ukosoaji huu haukuwa sahihi katika kipindi ambacho majeshi yetu yalikuwa yanahitaji kutiwa moyo na mtu anayewania kuwa Amiri Jeshi Mkuu. Tatu, katika moja ya mikutano yake ya hadhara mjini Shinyanga, Dk. Slaa aliwahi kutangaza kwamba aliyekuwa mkuu wa mkoa huo alikuwa amefariki. Hii ilikuwa ni baada ya kunong’onezwa na mke wake waliyekuwa naye jukwaani. Hali hiyo ilileta mshituko mkubwa kwa waliohudhuria mkutano huo pamoja na wanafamilia wa aliyekuwa Mkuu huyo wa Mkoa. Hii ilikuja kuthibitika kwamba ilikuwa ni uwongo na aliyezushiwa kifo na Dk. Slaa yupo hai hadi leo hii. Hii ni mifano michache ambayo inatia shaka kuhusu hekima na weledi wa Dk. Slaa. Aidha, kauli zake tata zimemwachia taswira ya kudumu kwamba ni mwanasiasa mwongo aliye tayari kuzusha lolote kwa maslahi ya kisiasa bila kujali hisia za watu wengine. Hitimisho Dk. Slaa anabebwa na taswira ya uadilifu. Hii ni taswira muhimu sana katika kampeni za mwakani kwa kuzingatia kwamba nchi imevimbiwa na ufisadi na itahitaji kiongozi jasiri anayeweza kupasua tumbo la ufisadi ili nchi ipumue. Katika hili, Dk. Slaa anabebwa na rekodi yake ya kutokuhusishwa na ufisadi wowote popote alipofanya kazi na ujasiri wake wa kuibua vitendo vya kifisadi popote na wakati wote alipovibaini. Pamoja na taswira hii njema, Dk. Slaa ana kazi ya kuuthibitishia umma kwamba yeye si tu mpiga mbinja, bali ni kiongozi anayeweza kudhibiti na kukomesha vitendo vya kifisadi. Kwa historia ya utendaji wake wa muda mrefu ndani ya CHADEMA hili ni eneo ambalo limemshinda. Dk. Slaa atakuwa na kazi ya kutetea uwezo wake wa kihekima na weledi katika maamuzi yake mbalimbali. Kwa mifano niliyoitoa hapo juu inaonyesha wazi kwamba ni mtu anayetumia zaidi hisia za moyoni katika kuamua mambo na hii inaweza ikawa hatari kwa kiongozi wa ngazi ya urais. Namtakia Dk. Slaa kila la heri katika harakati zake za kuwania kiti cha urais wa nchi yetu mwakani. Soma zaidi kuhusu: Urais 2015Slaa Tufuatilie mtandaoni TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
LIKE PAGE YETU HAPO PIA SHARE STORY NA RAFIKI ZAKO

0 comments:

Post a Comment

BURUDANI

 
Top