Mhe Zitto Kabwe
Kinyongo cha Mwalimu kwa NBC halali Zitto KabweToleo la 377 29 Oct 2014 MJADALA wa kuuzwa Benki ya NBC kwa bei ya kutupwa bado haujafa na haustahili kufa mpaka ukweli halisi ufahamike kwa umma. Ukweli kujulikana ni sehemu tu ya Taifa kukua na kujifunza makosa yaliyofanyika. Katika maandiko yangu kadhaa na hotuba zangu katika mikutano ya kisiasa, kitaaluma na hata bungeni nimekuwa nikisema kuwa Ubinafsishaji ni suala ambalo nchi yetu haijalifanyia kazi vya kutosha ili kutorejea makosa. Nikiwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC) tuliwahi kupendekeza mwaka 2009 kwamba Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) afanye uchunguzi maalumu kuhusu zoezi hili. Taarifa niliyonayo ni kwamba CAG amefanya kazi hii kwa Mashirika 10 yaliyouzwa na Taarifa amewasilisha kwa Kamati ya PAC. Hata hivyo, ubinafsishaji wa Benki ya NBC haukuwa sehemu ya uchunguzi huu. Kamati ya PAC, ambayo mimi ndiyo Mwenyekiti wake, inayoendelea na vikao jijini Dar es Salaam wiki hii ilikutana na Watendaji wa Ofisi ya Msajili wa Hazina ambaye ndiye mmiliki wa mali zote za Serikali kwenye Mashirika ya Umma au Kampuni binafsi ambazo Serikali ina hisa. Moja ya suala lililoibua mjadala ni uwezekano wa Serikali kupoteza hisa zake 30% katika Benki ya NBC. Hii inatokana na agizo la Benki Kuu la kutaka mtaji wa benki hiyo kuongezwa kufidia hasara kubwa ambayo NBC ilipata na hivyo kuchota akiba yake (reserves). Kwa kuwa Serikali haikuwa na fedha, iliamua kukopa kwa mbia mwenzake, Benki ya ABSA ya Afrika Kusini, jumla ya shilingi 22.5 bilioni kwa riba ya asilimia 8 kwa mwaka ili kuchangia mtaji wake ndani ya benki hiyo. Iwapo Serikali haitakuwa imelipa mkopo huo mpaka ifikapo Mwezi Machi mwaka 2015, his azote za Serikali katika NBC zitayeyuka (diluted). Mwanzo Ni muhimu kukumbuka kuwa NBC iliuzwa kwa jumla ya shilingi bilioni 15 kwa mujibu wa mkataba wa mauzo. Miniti za kikao cha iliyokuwa Tume ya Rais ya Kurekebisha Mashirika ya Umma (PSRC) za tarehe 20 Julai, 1999 zinaonyesha kuwa licha ya serikali kulipwa shilingi bilioni 15, kwa kuwa ABSA watakuwa wamelipa kwa fedha za kigeni (dola za marekani), basi pakiwa na faida yeyote ya mabadiliko (exchange gain) itakwenda ABSA. Faida hiyo ilitokea kwani shilingi iliporomoka mara baada ya mauzo hayo. Pia serikali ilitoa dhamana (bonds) za thamani ya shilingi bilioni 28 kama mtaji kwa benki hiyo. Zaidi pia, fedha ambazo ABSA waliilipa serikali zilitokana na fedha za iliyokuwa NBC katika mgawanyo wa hifadhi ya fedha kati yake na Benki ya Makabwela (NMB). Kimsingi, toka mwanzo kabisa, ABSA walipewa benki bure na wakapewa mtaji wa kuanzia kazi. Pia ABSA walipewa mkataba wa kuendesha benki na pia kusaini mkataba wa ufundi. Kila mwaka tangia mwaka 2000, jumla ya dola za kimarekani milioni saba zinakwenda Afrika Kusini kutoka NBC kama malipo ya gharama za uendeshaji na gharama za kiufundi. Akaunti zote za NBC zipo nchini Afrika Kusini. Suala hili, licha ya kusemwa sana, halijafanyiwa uchambuzi wa kutosha kwani ni suala ambalo linahitaji uchunguzi wa kijinai na hata adhabu kutolewa kwa wote waliohusika na uuzaji wa mali za umma kwa kiwango cha namna hii. Ifahamike kuwa kupinga uporaji sio kupinga mabadiliko ya kiuchumi. Kila nikipata fursa nasema, ‘privatization’ si sawa na ‘liberalisation’ isipokuwa la kwanza limo ndani ya la pili. Kwanini mtaji uliotolewa kwa ABSA kupitia ‘bonds’ za Serikali hawakupewa NBC? Kwa nini kama tatizo lilikuwa ni uwezo wa kuendesha, hatukukodisha menejiment tu? Sasa Kati ya mwaka 2005 na 2008, NBC walianza kutoa mikopo ya magari kwa sekta ya usafirishaji. Mikopo hii ilisababisha hasara ya zaidi ya shilingi bilioni 137 kwa benki hiyo na kwenye mahesabu ya benki hazikuwa zimeonyeshwa kuwa ni hasara (not provided for) kwa hiyo mizania ya benki ilikuwa inaonyesha mambo safi wakati kuna hasara. Zilipokuja kuwekwa kwenye mizania (imparement), hifadhi (reserve) ya Benki ikaliwa kwa jumla ya shilingi bilioni 50, Benki Kuu ikaingilia kati na kutoa agizo la kuongeza mtaji. Hiki ndio chanzo cha hali ya sasa kwamba kila mbia aweke fedha kulipia mtaji na serikali kuchukua mkopo kulipia mtaji huo. Masuala ya msingi ya kujiuliza ni: Mbia mmoja ni mwendeshaji na kaleta hasara kwa Benki. Ni kwa nini wabia wengine waumizwe na uendeshaji mbovu wa mbia mmoja? Huu mkataba wa uendeshaji hauna adhabu kwa mbia huyu mwendeshaji? Taasisi za uchunguzi wa jinai zilifanya uchunguzi kuhusu mikopo hii ya magari? Haya ni masuala ambayo hayana majibu ingawa kampuni iliyokuwa inatoa mikopo hiyo inajulikana na wakuu wa benki waliohusika na mradi wa hovyo namna hiyo wanajulikana na walipewa bonus zao na kurudi Afrika Kusini. Kamati ya PAC imeagiza mapitio ya mkataba wa mauzo wa Benki na mkataba wa msaada wa kiufundi. Hata hivyo kwa hali ilivyo kuna mengi ndani ya NBC hatuyajui na tunapaswa kuyajua. Kwa wanazuoni, tunaweza kujifunza makubwa zaidi kama mtu akifanya utafiti wa kitaaluma kuhusu kuuzwa kwa Benki ya NBC. Kwa vyovyote vile, Mwalimu Julius Nyerere alikuwa na sababu ya kuwa na nongwa kuhusu suala hili. Alijua tusiyoyajua. Soma zaidi kuhusu: Mwalimu NyerereNBCABSAPAC TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
0 comments:
Post a Comment