Dereva wa pikipiki aliyefahamika kwa jina moja la Temba anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 25 hadi 35 amenusrika kupoteza maisha akiwa na mteja wake baada ya kugongwa na gari la kampuni ya ulinzi la Security Group Africa mjini Moshi mapema leo.
Tukio hilo limetokea majira ya 2:45 asubuhi katika barabara ya Boma Road mjini Moshi likihusisha bodaboda yenye namba za usajili T 587 CYR aina ya boxer na gari lenye usajili nambari T 708 BAF aina ya Nissan
Gari hilo la kampuni la ulinzi lilikuwa likiendeshwa na dereva aliyefahamika kwa jina la Leornad Essau (34) aliyekuwa akitokea mzunguko wa Arusha kuelekea Voda House mjini humo.Mashuhuda wa tukio hilo walisema gari hilo la ulinzi lilikuwa mwendo kasi mbele yake kulikuwa na bodaboda ilikyokuwa ikimwonyesha ishara ya kupinda kulia ikitokea upande wa kushoto ndipo ilipomgonga kwa nyuma na kusababisha ajali hiyo.

Mashuhuda hao waliongeza kusema madereva wa kampuni hilo wamekuwa na tabia ya kukimbiza magari yao pasipo kuwa na sababu za msingi ikiwemo kuwahi kunywa chai na mihogo ambayo hupikwa karibu na eneo la Voda House.

“Yaani hawa madereva kila siku asubuhi wamekuwa na mashindani kama ya magari (motor rally), unafikiri wanawahi tukio fulani kumbe wala, ni kuwahi kunywa chai na mihogo hapo voda house” alisema shuhuda mmoja.

Dereva wa Bodaboda alikimbizwa katika hospitali  ya KCMC kwa matibabu zaidi huku abiria wake mwenye jinsi ya kike (anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 22 hadi 30) akikimbizwa katika hospitali ya Kilimanjaro kwa matibabu zaidi.

Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki na Waendesha bodaboda mkoa Kilimanjaro (CWBK) Bahati Nyakiraria alisema madereva wengi hawana udereva wa kujihami kama ambavyo sheria inawaagiza kufanya hivyo.

Hata hivyo aliongeza kusema madereva wa bodaboda wamekuwa wakionewa kuwa ni wavunjaji wa sheria za usalama barabarani kumbe wakati mwingine wenye magari ndio wamekuwa wakisababisha ajali zinazoweza kuzuilika.

Maafisa wa Jeshi la Polisi walionekana katika eneo la tukio wakiendelea na utaratibu wao wa kupima chanzo cha ajali hiyo.












TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
LIKE PAGE YETU HAPO PIA SHARE STORY NA RAFIKI ZAKO

0 comments:

Post a Comment

BURUDANI

 
Top