Inspekta Jenerali wa Polisi, Ernest Mangu


Sumbawanga. Watu wasiofahamika wamemvamia na kumuua mganga wa kienyeji, Salehe Garimoshi (65), mkazi wa Kijiji cha Milala wilayani Mpanda kwa kumpiga  risasi kichwani kisha kuukatakata mwili wake kwa mapanga.
Taarifa kutoka eneo la tukio, zilizothibitishwa na Jeshi la Polisi zinadai kuwa baada ya mganga huyo kuvamiwa na  watu hao, mmoja wao  aliyekuwa na bunduki, alimfyatulia  risasi kichwani kisha kuamuru wenzake wamkatekate kwa mapanga.
Kaimu kamanda wa polisi wa Mkoa wa Katavi, Focus Malengo alisema jana kuwa mauaji  hayo yalitokea  Agosti 10, saa  2:00 usiku, wakati mganga huyo alipokuwa anakula na familia.
Kabla ya mauaji hayo, inadaiwa kwamba siku hiyo mchana, watu wawili  walifika  nyumbani  kwa mganga  huyo na kumkuta Peter Martin  aliyekuwa anaishi nyumbani hapo kwa ajili ya kupata tiba ya ugonjwa uliokuwa unamsumbua.
Kamanda alisema watu hao walimuuliza Martin kama mganga huyo yupo na kujulishwa kuwa hakuwepo.
“Hapo ndipo watu hao walipoamua kumpigia simu mganga  huyo na kumjulisha kwamba wapo  nyumbani kwake, wanahitaji  kumuona ili awasaidie.  Muda mfupi  baadaye mganga alifika na kuwakuta watu hao ambao walimwambia mganga kuwa wana mgonjwa, lakini wamemwacha mbali kwa sababu gari lililombeba  limeharibika  katika Kijiji cha Kakese, hivyo watamleta baadaye,” alisimulia kamanda Malengo na kuongeza kwamba mganga  huyo aliwakaribisha watu hao chakula cha mchana.
Inadaiwa ilipotimu  saa 12:00 jioni, wageni hao wawili walidai kwamba wanamfuata mgonjwa wao na kuahidi kurejea nyumbani kwa mganga huyo saa 2:00 usiku.
Kamanda Malengo alisema ilipofika muda huo, mganga huyo, familia yake na wagonjwa waliokuwa wanatibiwa wakiwa wanakula chakula usiku, nje ya nyumba,  ghafla  walifika watu wanne kati yao wawili ni wale waliokuwa wameaga kuwa wanakwenda kumleta mgonjwa.
Alisema mmoja kati ya  watu hao alimwambia mganga amtazame usoni,  kisha akampiga  risasi kichwani na kuwaamuru wenzake wamkatekate kwa mapanga mganga huyo kisha wakatoweka.
Alisema uchunguzi wa polisi  bado  unaendelea na hadi  sasa  chanzo  cha mauaji  hayo  hakijafahamika TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
LIKE PAGE YETU HAPO PIA SHARE STORY NA RAFIKI ZAKO

0 comments:

Post a Comment

BURUDANI

 
Top