TUJIUNGE NYUMBANI KWA RAY C
Ilidaiwa kuwa tukio hilo lilitokea usiku wa kuamkia Alhamisi iliyopita
nyumbani kwa Ray C, Changanyikeni jijini Dar es Salaam ambapo
ilisemekana kwamba Chid Benz alimvamia mishale ya saa 4:00 usiku kwa gia
ya kumsaka mzazi mwenzake aliyemtaja kwa jina moja la Mariam.
CHID BENZ ATAKA KUMUONA MWANAYE
Ilidaiwa kwamba Chid Benz alisema kuwa alizungumza na mpenziye huyo
kwamba alitaka kwenda kumuona mwanaye ambapo Mariam alimjibu kwamba kwa
muda huo alikuwa nyumbani kwa Ray C Changanyikeni.
UNGA WATAJWA
Sosi wetu alidai kwamba baada ya kujibiwa hivyo, Chid Benz alianza
kulalama na kumwambia anamfuata palepale kwa nini usiku ule alale kwa
Ray C, wakati ana uwezo wa kwenda nyumbani au amekwenda kwa staa huyo
ili kunywa dawa zao za kuondoa sumu ya madawa ya kulevya ‘unga’, jambo
ambalo jamaa huyo siku zote huwa hataki hata kulisikia masikioni mwake.
CHID BENZ AWAVAMIA
“Huwezi kuamini baada ya muda kama wa saa moja, Ray C na Mariam wakiwa
ndani wakitazama TV, ghafla mlango ulisukumwa kwa nguvu kisha akaingia
Chid Benz na kumdaka Mariam na kuanza kumshushia kipigo.“Yaani huo
mshtuko walioupata walidhani wamevamiwa na Al-Shabaab.
KIBAO CHAMGEUKIA RAY C
“Mungu mkubwa kwa sababu Mariam alifanikiwa kuchoropoka na kukimbilia chumbani ndipo kibao kikamgeukia Ray C.
“Ray C akiwa anashangaa ghafla naye alipokea kipigo kikali kutoka kwa Chid na kumsababishia majeraha mbalimbali mwilini.
RAY C AKIMBILIA KWA MAJIRANI
“Baada ya kuona maji yanazidi unga, Ray C alitafuta upenyo na kukimbilia
kwa majirani huku akipiga kelele za kuvamiwa, mara moja majirani
waliambatana naye mpaka nyumbani kwake.
“Walipofika Chid Benz alikuwa ametumia staili za kininja kwa kuruka geti
na kutokomea kusikojulikana huku akiwaacha Ray C na Mariam wakiangua
vilio kwa kipigo kikali walichopokea.
RAY C AVUJA DAMU
“Ray C aliumia mkono na mguu ambao ulionekana ukivuja damu. Mariam
alikuwa akililia mbavu zake kuchakazwa kwa makonde mazito na upande
mwingine baadhi ya vyombo vya ndani vikionekana kuvunjwa na vingine
kusambaratishwa kufuatia tafrani iliyozuka muda mfupi baada ya Chid Benz
kutia maguu nyumbani hapo,” chanzo kilishusha madai hayo mazito.
RAY C ATIRIRIKA SAKATA LILIVYOKUWA
Akizungumzia na gazeti hili Alhamisi iliyopita juu ya sakata hilo, Ray C
alisimulia mkasa mzima: “Kweli Chid Benz alikuja nyumbani kwangu na
kunivamia.
“Alinipiga vibaya sana na kuvunja baadhi ya vitu vya ndani kwangu, jambo
ambalo lilinishangaza zaidi ni namna alivyopafahamu nyumbani kwangu
hadi kuja kunifanyia fujo nikiwa na mzazi mwenzake, Mariam ambaye
nilitoka naye ofisini kwangu.
“Ujue jana (Jumatano) tulikuwa na kazi sana ofisini kwangu mimi na
Mariam, sasa kutokana na kubanwa na kazi kweli muda ulienda sana hivyo
nikamwambia Mariam akalale kwangu.
“Kwa kuwa muda ule ilikuwa ngumu kwenda kwao Mbezi Beach, Mariam alikubali na tulikwenda wote nyumbani kwangu.
“Huko nyuma Mariam alikuwa mwathirika wa madawa ya kulevya lakini baada
ya kusikia mimi nimeacha, naye aliachana nayo na kuanza kutumia dawa za
kuondoa sumu.
“Tumeendelea kutumia naye dawa na sasa ameshapona kabisa hivyo kuna
baadhi ya kazi nimekuwa nikimshirikisha kunisaidia kwenye ofisi yangu.
Pia alishawahi kumshawishi Chid Benz ili aje kutumia dawa lakini jamaa
alikataa na kumfanyia vurugu sana huku akimkataza kuwa na mimi kwa madai
mimi ndiyo namfanya amwambie kuachana na utumiaji dawa za kulevya.
“Sasa jana alipojua hivyo nadhani Chid Benz alikuja kutimiza dhamira yake ambayo siku nyingi alikuwa akiahidi kunipiga.”
SOO LIPO POLISI
Ray C alisema baada ya tukio hilo alikwenda kuripoti kwenye Kituo cha
Polisi cha Oysterbay, Kinondoni na kufunguliwa jalada la kesi ambapo
Chid Benz anasakwa na polisi.
Juhudi za kumpata Chid Benz hazikuzaa matunda kwani simu yake haikuwa
hewani hivyo jitihada zinaendelea na kama ana ufafanuzi au utetezi
anaweza kutupigia.
CHID BENZ NI TATIZO?
Chid Benz anadaiwa kuwa ni tatizo kwani tukio hilo la Ray C amelifanya
wakati akiwa na tukio la pili kwa wanawake kwani kwenye Mahakama ya
Mwanzo, Ilala ana kesi mbichi aliyoshitakiwa kwa kosa la kumpiga mrembo
aitwaye Mwanaisha.
Mbali matukio hayo pia Chid Benz ana rekodi ya kukorofishana na wasanii wenzake kama Kalapina na marehemu Ngwea.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
0 comments:
Post a Comment