Lile
sakata la utekaji na upoteaji wa watoto ambao wengi ni wanafunzi wa
shule za msingi katika Jiji la Dar na kudaiwa linafanywa na watu walio
kwenye magari aina ya Toyota Noah limeingia katika sura nyingine.
Safari
hii, gari moja lilitupiwa mawe na dereva nusura kuuawa kufuatia kufika
katika Shule za Msingi za Kombo na Mtakuja zilizopo Vingunguti, Dar kwa
lengo la kuzungumza na walimu kuhusu mikopo lakini likahofiwa lilikwenda
kuteka watoto.
Tukio
hilo lilijiri Ijumaa iliyopita na kusababisha vurugu kubwa kati ya
wazazi na walimu hali iliyowafanya maafande wa Kituo cha Polisi Buguruni
kuwasili katika eneo la tukio ili kutuliza ghasia na kwanusuru walimu.
Uwazi
lilifika eneo la tukio muda mfupi na kuwakuta walimu wakiwa chini ya
ulinzi wa polisi ili wasishambuliwe na wazazi ambao walivamia shule
wakidai kwamba watoto watatu walitekwa na watu wenye Noah jeusi.
Vurugu
hizo zilizoanza saa nne asubuhi siku hiyo zilitokea baada ya gari moja
jeusi aina ya Toyota Noah kufika shuleni hapo na kushambuliwa na
wananchi wakidai kwamba ndilo linalotumika kuwatekea watoto wao shuleni
hapo.
Mmoja
wa wazazi aliyejitambulisha kwa jina la Huma Selemani alisema Noah hilo
la mikopo kwa walimu lililokuwa na vioo vyeusi lilihisiwa ni la utekaji
baada ya jana yake (Alhamisi) ambapo gari kama hilo lilifika shuleni
hapo na dereva kumuuliza mmoja wa wanafunzi sehemu hiyo inaitwaje ambapo
mwanafunzi huyo alisema haijui.
Ilidaiwa
kuwa, pamoja na denti huyo kusema haijui sehemu hiyo walimchukua na
kumuingiza ndani ya gari hilo ili kuondoka naye lakini mzazi mmoja
aliona na kupiga kelele huku akilishambulia kwa mawe gari hilo hadi
walipomshusha mwanafunzi huyo na wao kutimka.
Mayowe
hayo yaliwafanya wazazi kuvamia shule hizo na kusababisha wanafunzi
kutoka madarasani huku wengine wakiruka ukuta na kukimbilia majumbani na
baadhi kwenda kusikojulikana.
Wazazi
waliokuwa karibu na shule hizo walifika na kuwachukua watoto wao kisha
kwenda nyumbani huku wengine wakitegemea msaada toka polisi ambao
walipofika walifyatua risasi hewani kuwatawanya wananchi hao.
Hata
hivyo, walimu wakuu wa shule hizo hawakupatikana mara moja lakini
mwalimu mmoja ambaye hakupenda jina lake liandikwe alisema hakuna
utekaji wa watoto shuleni bali baadhi ya watu wamekuwa wakivumisha
habari hizo na hivyo kuwatia hofu watoto.
Baadhi
ya watu walioongea na Uwazi walisema kuwa, wana taarifa mbaya kwamba
watekaji hao wakishawapata watoto huenda kuwaua ili kutwaa viungo vyao
kwa ajili ya ushirikina wa kupata utajiri.
Mwenyekiti
wa Serikali ya Mtaa wa Kombo, Jastin John Chiganga alipohojiwa alikiri
kutokea kwa vurugu hizo hali iliyomfanya awaite polisi kutuliza ghasia
lakini alisema kwa upande wa kutekwa watoto na gari aina ya Noah
hajawahi kusikia.
“Shule ilibidi ifungwe, watoto waruhusiwe kutawanyika hadi hapo taarifa itakapotolewa. Hata hivyo, wazazi wameniomba kwamba kabla watoto wao hawajarejea shuleni hapo anatakiwa kiongozi wa juu, awe DC (mkuu wa wilaya) au yeyote afike kutoa tamko na kuweka mambo ili kuwatoa hofu wazazi na wanafunzi,” alisema mwenyekiti huyo.
Polisi
wa Buguruni waliokuwepo kwenye tukio hilo walisema hawana taarifa ya
watu waliojeruhiwa au kukamatwa bali zoezi la kudhibiti amani
lilifanyika kwa uangalifu wa hali ya juu.
Wakati
huohuo, wazazi wa mwanafunzi Hadija Hansi (10) anayesoma darasa la nne
Shule ya Msingi Magomeni, Dar wanahaha kumtafuta mtoto wao huyo ambaye
alitoweka katika mazingira ya kutatanisha ikidaiwa alitekwa na Noah.
0 comments:
Post a Comment