Jaji mstaafu Joseph Warioba

Aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Kuratibu Maoni  ya Katiba, Jaji Mstaafu Joseph Warioba, ameitega serikali kwa kuitaka kusambaza kwa wingi Rasimu ya Katiba inayopendekezwa na Bunge Maalum la Katiba (BMK) ili wananchi waisome na kufikia maamuzi sahihi.

Hatua hiyo imekuja wiki moja baada ya Jaji huyo kutangaza msimamo wake wa kuipinga Rasimu hiyo, wakati wa maadhimisho ya kutimiza miaka 19 ya Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC).



Jaji Warioba alitoa kauli hiyo kufuatia BMK kuvunjwa rasmi jana baada ya kumaliza kazi yake ya kupitia Rasimu ya Pili ya Katiba.
Rasimu inayopendekezwa inatarajiwa kukabidhiwa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete na Rais wa Zanzibar, Dk. Mohamed Ali Shein, Jumatano ijayo, mjini Dodoma.

Katika mahojiano maalum na NIPASHE Jumapili jana baada ya Rasimu hiyo kupitishwa, Jaji Warioba alisema: “Mchakato ulifanyika kwa awamu ya kukusanya maoni, tukaja BMK lililomaliza kazi yake juzi na sasa tunaelekea kwa wananchi, naiomba serikali itoe nakala nyingi za rasimu ili wananchi waisome, waielewe na wajue nini cha kufanya dhidi ya hatma ya nchi yao,” alisema.

MAMBO MUHIMU YALIYOINGIZWA
Kuhusu Rasimu ya BMK, Jaji Warioba alisema yapo mambo muhimu yameingizwa ambayo yanalenga kuleta mabadiliko.

“Mengi ni yale yaliyopendekezwa na Tume,  malengo muhimu ya taifa Bunge hili imeyapitia na kuyarekebisha na kutoka na malengo mazuri ya kisiasa, kiuchumi,  kijamii, kitamaduni na kimazingira,” alisema.

Aidha, alisema suala la haki za binadamu Tume iliyaangalia na BMK imeyarekebisha.

“Kuhusu madaraka ya rais, bunge limependekeza uteuzi wa viongozi muhimu kama wajumbe na mwenyekiti wa tume muhimu kama haki za binadamu sasa rais anashauriwa, anateua kutokana na ushauri anaopewa mahali pengine kuna kuwa na kamati za  ushauri,” alisema.

YALIYOONDOLEWA
Jaji Warioba alisema ushauri wao kuhusu viongozi wanaotakiwa kuthibitishwa na Bunge, BMK wamebakiza Waziri Mkuu.

“Kwa ujumla madaraka ya Rais yamepunguzwa kwa kiwango, maeneo mengine ambayo bado tuna wasiwasi baadhi ni mgombea binafsi, rasimu imetaja sifa ambazo mtu anayetaka kugombea, miongoni ni awe raia, kujua kusoma na kuandika, kifungu hicho kinasema sheria itatungwa na kufafanua zaidi,” alisema.

Jaji Warioba alifafanua kuwa BMK imeweka masharti zaidi kwa mgombea binafsi aeleze lini ametoka kwenye chama cha siasa, idadi ya watu wanaomdhamini, utaratibu wa kuainisha vyanzo vya mapato.

Katika kipengele hicho, Jaji Warioba alionyesha wasiwasi wake kuhusu masharti hayo na kuhoji kwa nini yasihusishe wagombea wote.

“Masharti haya yanafanywa yawe magumu ili mtu asigombee, yalipaswa kuwa kwenye Sheria ya Uchaguzi na siyo kwenye katiba, huku ni kumbana mgombea binafsi,” alisema.

MUUNGANO
Aidha,  alisema katika suala la Muungano moja ya kero ni uhusiano wa mambo ya fedha katika Katiba ya sasa.

“Lakini tangu mwaka 1977 Zanzibar ilikataa na sababu zinajulikana, kuna mambo yanasimamia kuiendesha Zanzibar na yanahitaji fedha na vyanzo vikubwa vya fedha ni kodi,”alisema na kuongeza:

Sisi tulijiondoa kwenye mambo ya muungano na kubakiza ushuru wa bidhaa, kwa sababu mapato makubwa yanatokana na kodi na ushuru wa forodha, sasa kama wamerudisha iwe ya muungano na kuminywa uwezo wa kifedha, nashangaa kama wazanzibar wamekubali hili kwa kuwa halitatekelezwa kama mwaka 1977,” alisema.

Jaji Warioba alionyesha wasiwasi katika suala hilo na kueleza kuwa endapo halitatekelezwa wataingia kwenye mgogoro mwingine na kusema wazanzibar hawachangii.

“Kutekeleza yaliyopitishwa na BMK maana yake Zanzibar ibadili Katiba yake, nina wasiwasi haitabadili kwa sababu kuibadili ni lazima kuwe na maridhiano kati ya makundi makubwa ya Zanzibar na mengine,” alisema.

Alisema jinsi alivyokuwa akifuatilia lugha zilizozungumzwa, haoni kama kuna maridhiano kwa kuwa kwenye Baraza la Wawakilishi ni lazima theluthi mbili zipatikane.
Alifafanua kuwa ndani ya BMK ilikuwa rahisi kupatikana kwa theluthi mbili kutokana na wajumbe wa kundi la 201.

Jaji Warioba aliongeza kuwa kwa upande wa Zanzibar haoni kama kutapatikana maridhiano ikiwa Katiba yao haitabadilishwa.

“Hii itafanya matatizo ya muungano kubaki pale pale, kazi kubwa ipo Zanzibar na mafanikio yao ndiyo yataleta mafanikio ya rasimu hii, kusipokuwa na maridhiano katiba hii haitaweza kutekelezwa,  pia lugha za viongozi wa Zanzibar ni za kuwatenganisha,” alisema.

UKAWA
Mkuu wa Idara ya Mawasiliano ya Chadema, Tumaini Makene, aliliambia gazeti hili kuwa, viongozi wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), wanaendelea na mazungumzo na wakati wowote watatoa msimamo wao dhidi ya BMK.

“BMK ambalo kimsingi lilikuwa sawa na mkutano mkuu wa CCM na mawakala wake limetumia njia tunazoziita za kiharamia ili kupata theluthi mbili kupitisha katiba isiyotokana na maoni ya wananchi,” alisema na kuongeza:

“Limetangaza mgogoro chanya na mwanya mwingine wa agenda kubwa ya kuwaunganisha Watanzania kupigania mabadiliko ya kweli dhidi ya maharamia wa demokrasia na maoni ya wananchi,” alisema.

Makene alisema kuwa, vikao vya kamati ya ufundi na viongozi wakuu vinaendelea na vitakapokamilika watawaeleza Watanzania matarajio na msimamo wao.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
LIKE PAGE YETU HAPO PIA SHARE STORY NA RAFIKI ZAKO

0 comments:

Post a Comment

BURUDANI

 
Top