.
Kesi ya mwanafunzi wa darasa la tatu (jina linahifadhiwa) katika Shule ya Msingi Ukombozi iliyofunguliwa katika Kituo cha Polisi cha Urafiki, jijini Dar es Salaam baada ya kudaiwa kulawitiwa imefutwa.
Kesi hiyo ambayo ilifunguliwa Septemba 15, mwaka huu kituoni hapo, ikimkabili mtuhumiwa aliyetajwa kwa jina moja la Enock, imefutwa jana na mtu huyo kuachiwa huru kwa madai kuwa, imekosa ushahidi.
Mama wa mtoto huyo (jina linahifadhiwa), aliliambia gazeti hili kuwa, mpelelezi wa kesi hiyo aliyemtaja kwa jina moja la Suzana aliiambia familia hiyo kuwa, baada ya jalada la kesi kupelekwa kwa mwanasheria na kulipitia, alikosa ushahidi wa kulipeleka shauri hilo mahakamani.
Alisema baada ya kuripoti tukio hilo kituoni hapo alipewa RB/Urafiki/7627/2014.
Aidha, mama huyo alisema mjomba wa mtoto alipofuatilia kesi hiyo jana kituoni hapo alirudi na majibu kuwa imefutwa.
Alisema kuwa baada ya kukutana na mpelelezi wa kesi hiyo, alimweleza kuwa jalada la kesi limerudi kutoka kwa mwanasheria na mtuhumiwa anaachiwa huru kutokana na kukosekana ushahidi.
Alisema baada ya maelezo ya mpelelezi, aliomba kuonana na Mkuu wa Kituo hicho, ambaye naye alimweleza kuwa, majibu ya daktari yalionyesha hajalawitiwa.
Pia alisema mkuu huyo wa kituo alimweleza kuwa alichokieleza mtoto kuhusu mazingira ya nyumbani kwa mtuhumiwa yalikutwa tofauti.
Siku ya tukio mtuhumiwa huyo alikamatwa baada ya mama kuambatana mtoto wake siku ambayo kijana huyo alikuwa na miadi ya kukutana na mwanafunzi huyo.
Kabla ya kukamatwa kwake, kijana huyo ilidaiwa alishamfanyia vitendo hivyo mtoto huyo zaidi ya mara moja na alikuwa akimpa fedha kati ya Sh. 2000 na Sh. 7000 lakini siku ya kukamatwa alimpa Sh. 200.
Awali, Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Biamina Swai, aliliambia gazeti hili kuwa, kwa mwaka huu jumla ya matukio manne ya watoto kufanyiwa vitendo hivyo yalitokea lakini hilo moja ndilo mtuhumiwa wake alikamatwa baada ya kushirikiana na mzazi wake.
Alisema matukio mengine baada ya wazazi kupewa taarifa za ulawiti wa watoto wao, pindi waendapo mitaani huvujisha siri na kusababisha wahusika kukimbia TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
0 comments:
Post a Comment