Wiki iliyopita,wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba walianza kujadili ibara zilizojadiliwa katika kamati za bunge,ndipo Watanzania walipoanza kung'amua jinsi rasimu halisi ilivyochanwachanwa. Wengi wa wajumbe,husuan wale walioonja 'utamu' wa bunge la Jamhuri ya Muungano,wametupa mapendekezo ya wananchi yaliyoisukuma Tume ya Jaji Warioba kuelekeza kiwango cha elimu anachostahili kuwa nacho mbunge.

Tume ilizingatia maoni ya wananchi kwamba miongoni mwa sifa za mwananchi kugombea ubunge,iwemo ya kujua kusoma na kuandika lugha ya Kiswahili au Kiingereza.Pia awe mwenye elimu ya kiwango kisichopungua kidato cha nne.

Kamusi ya Kiswahili inasemaje kuhusu neno "boresha." Inataja, : "kuboresha" ni kitendo cha kuliongezea "jambo" umuhimu na uzito kutokana na lililopendekezwa au kutendeka awali.

Wajumbe wa Bunge Maalumu linaloongozwa na mwenyekiti Samwel Sitta,wamekuwa wakijinasibu kuwa kazi wanayoifanya siyo kuichanachana rasimu ya wananchi bali ni "kuiboresha."

Ninapovaa uhusika wa mwalimu wa darasa la nne,nawataka wanafunzi wangu waboreshe sentensi au wakiona inafaa waiache ilivyo: "Kujua kusoma na kuandika lugha ya Kiswahili au Kiingereza" na awe na "elimu isiyopungua kidato cha nne."

Natumaini nusu ya wanafunzi watajibu hivi: "Kujua kusoma na kuandika lugha ya Kiswahili au Kiingereza" na awe na "elimu isiyopungua kidato cha nne au cha sita."

Na nusu iliyobaki watjibu, "Kujua kusoma na kuandika lugha ya Kiswahili au Kiingereza" na awe na "elimu isiyopungua shahada ya chuo kikuu."

Naam hapo,wanafunzi wangu wote, "wameboresha" lakini wale wajumbe walioko Dodoma wanaikata sentensi hii na kuiacha nusu ikisema: "Kujua kusoma na kuandika lugha ya Kiswahili au Kiingereza."

Hivi hao kweli wanaweza kujigamba kuwa wameboresha? Na sio kwamba wamevuruga sentensi?

Ni mtanzania yupi wa zama hizi anayejua kusoma na kuandika vizuri Kiswahili na Kiingereza bila ya kuwa amepata elimu ya sekondari,na tena sekondari yenyewe ya kiwango?

kama mbunge si lazima awe na kiwango cha elimu cha kuridhisha katika dunia ya leo iliyojaa maendeleo ya sayansi na teknolojia akianzia na kujua kusona na kuandika Kiswahili na kiingereza, basi kesho itaelezwa kuwa madiwani na wenyeviti wa mitaa na vijiji si lazima wawe wanaojua kusoma na kuandika lugha ya taifa.

Inanikumbusha mtu aliyewahi kuwa Diwani wa kata fulani Wilaya ya Hanang',mkoani Manyara ambaye alilalamikiwa kwa kutojua kusoma wala kuandika ingawa alichaguliwa na wananchi.

Nikamsikia mjumbe wa Bunge Maalumu la Katiba akijitahidi kujenga hoja ya kutetea elimu ya mtu mwenye sifa za kuwa mbunge,huku akisisitiza umuhimu wa mawaziri kupaswa kutokana na wabunge kinyume na mapendekezo ya wananchi kupitia Tume ya Warioba. Alisema,"Wale wanaotaka mawaziri wasitokane na wabunge,wanasahau kuwa Rais ana nafasi 10 za uteuzi wa wabunge.Ikitokea wabunge wote wanajua tu kusoma na kuandika bila sifa ya ziada,basi mawaziri watatokana na wasomi watakaoteuliwa na Rais.

Haya yanatokea chini ya usimamizi wa Samwel Sitta yule mtaalamu wa viwango na kasi. Hapa kila mtu anajiuliza je,hivi ndivyo wenzetu wanavyoboresha Rasimu ya Katiba mpya inayotakiwa Watanzania wairidhie?

Kumbe sasa elimu haina umuhimu tena kwa utekelezaji wa mambo ya Watanzania? Kwamba mtu akiwa maarufu au mwenye fedha nyingi za kuweza kutambuliwa mheshimiwa inatosha?

Haya yakawa na ushiriki wa mwananchi anayeitwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali? Ajabu ya mwaka; uchakachuaji wa staili hii? Huyu si ndiye kila siku anawasilisha miswada bungeni ya marekebisho ya sheria au ya sheria mpya zilizoandikwa kwa Kiingereza,lakini 'ameuchuna' wajumbe wakichuana?

Haya Jaji wetu Werema,kama mambo haya yatapitishwa,tafadhali waeleze mapema wataalamu wako wajiandae kutayarisha miswada yote itakayowasilishwa bungeni kwa lugha nyepesi,tena ya Kiswahili chetu kitukufu.

Iwe hivyo maana Watanzania wanaaminishwa kuwa Tanzania ya leo haihitaji watendaji na watunga sera na sheria wenye weledi unaopaa kiwango! TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
LIKE PAGE YETU HAPO PIA SHARE STORY NA RAFIKI ZAKO

0 comments:

Post a Comment

BURUDANI

 
Top