SIKU
moja baada ya Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(Chadema), Freeman Mbowe, kuwekewa pingamizi la kutogombea nafasi hiyo
kwa awamu ya tatu, Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi,
amesema kinachotokea kwenye chama hicho ni matokeo ya kupuuza ushauri
wake.
Mbowe
amewekewa pingamizi na aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Tabora,
Kansa Mbarouk, ambaye pia ni mgombea wa nafasi hiyo, kwa madai ya
kukiuka katiba ya chama hicho na maagizo ya msajili wa vyama vya siasa.
Akizungumza
na MTANZANIA jijini Dar es Salaam jana, Jaji Mutungi alisema kuwa ofisi
yake iliwashauri viongozi wa chama hicho kuitisha mkutano wa Kamati Kuu
ili waweze kufanya marekebisho ya Katiba yao kabla ya uchaguzi, lakini
walipuuza ushauri wake.
Alisema kuwa baada ya ushauri wake huo kupuuzwa, Mbarouk ameona fursa hiyo na kuamua kuitumia.
“Tuliwashauri
Chadema muda mrefu kuitisha mkutano wa Kamati Kuu ili wafanye
marekebisho ya Katiba yao, lakini walitupuuza na kuanza kutulaumu.
Kinachotokea sasa ni matokeo ya kile ambacho tulijua kinaweza kutokea
katika uchaguzi wao,” alisema Jaji Mutungi.
Alisema baada ya kuwaambia hayo, viongozi wa chama hicho waliishutumu ofisi ya msajili na kudai kuwa inatumika.
Jaji
Mutungi alisema kutokana na hali hiyo, ofisi yake imeamua kukaa kimya
na kuacha mchakato wa uchaguzi uendelee, lakini mwishowe wanatakiwa
kuwasilisha taarifa zao katika ofisi hiyo.
“Tumeamua kuwaacha waendelee na mchakato wao, watavutana mwisho watachoka wakimaliza watatufuata,” alisema.
Mbarouk
aliwasilisha taarifa yenye kumbukumbu namba Mbarouk/UCH/14 kwenda kwa
Katibu Mkuu wa Chadema na Msajili wa Vyama vya Siasa ambayo inasema kuwa
kufikia Septemba 14, siku ya uchaguzi mkuu wa chama hicho, Mbowe
atakuwa ametumikia vipindi viwili katika nafasi ya mwenyekiti taifa.
Kulingana
na Katiba ya Chadema kama ilivyothibitishwa na Msajili wa Vyama vya
Siasa, hakuna mwanachama anayeruhusiwa kuchaguliwa kuongoza zaidi ya
vipindi viwili katika cheo kimoja na ngazi moja.
Juni
mwaka huu, msajili alidai kuwa Mbowe hawezi kuwania nafasi hiyo
kutokana na Katiba yao kuwa na kipengele cha ukomo wa uongozi wa vipindi
viwili.
Alisema
ili aweze kuendelea na nafasi hiyo, alipaswa kuitisha mkutano wa Kamati
Kuu ili waweze kufanya marekebisho katika Katiba yao ikiwa ni pamoja na
kuondoa kipengele cha ukomo wa uongozi.
Katika hatua nyingine, chama hicho kimesema hakijapata taarifa za Mbowe kuwekewa pingamizi.
Akizungumza
na waandishi wa habari katika ofisi za chama hicho jana, Mkurugenzi wa
Kampeni na Uchaguzi, Singo Benson, alisema kulingana na Katiba ya chama
hicho walioomba kuteuliwa kama wana pingamizi au malalamiko wanapaswa
kupeleka ofisini, lakini hawajapokea hadi sasa.
“Sisi
tumesoma tu kwenye magazeti, hatuna taarifa yoyote ya pingamizi hadi
sasa. Huyo anayesema alileta je, alilileta kwa njia gani na kama
‘dispatch’ ipo, aseme nani alipokea na kusaini,” alisema Benson.
Alisema
ofisi ya chama hicho iko wazi muda wote na kwamba kwa siku ya juzi
alikuwapo ofisini hadi saa 5 usiku, lakini hakupokea pingamizi la aina
yoyote.
Wakati huo huo, chama hicho jana kiliwatangaza washindi wa uchaguzi wa Baraza la Wazee Taifa.
Nafasi
ya mwenyekiti ilichukuliwa na Hashim Juma Issa kutoka Zanzibar, Makamu
Mwenyekiti Bara ni Suzan Lyimo na Makamu Mwenyekiti Zanzibar ni Omar
Masoud Omar.
0 comments:
Post a Comment