Hatua
ya Rais Mstaafu, Benjamin Mkapa, kujiweka kando kuzungumzia suala la
mchakato wa Katiba Mpya na mwenendo wa Bunge Maalum la Katiba, imeibua
maoni tofauti ya wananchi huku baadhi wakisema anakosea na wengine
wakimtetea kwa maelezo kuwa uamuzi huo ni matokeo ya busara ya hali ya
juu aliyo nayo.
Mhadhiri
wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine (Saut), Profesa Mwesiga Baregu,
alisema inashangaza kwa Mkapa kukwepa kuzungumzia suala la mchakato wa
katiba wakati inafahamika ni kiongozi mwenye msimamo.
Prof.
Baregu ambaye alikuwa Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, alisema
taarifa zilizopo ni kwamba ndani ya chama chake cha CCM, Mkapa alifanya
ushawishi mkubwa kupendekeza muundo wa serikali mbili uwe ndiyo msimamo
wa chama hicho na kupinga mapendekezo yaliyotolewa na Tume ya Mabadiliko
ya Katiba ya serikali tatu.
“Mkapa
ndiye mwasisi wa suala la uwazi, lakini sijui kwa nini uwazi unamshinda
katika suala hili. Sijui alivyostaafu ndiyo uwazi nao ukaishia hapo,” alisema.
Alisema
Mkapa kama kiongozi mkuu mstaafu wa nchi, anawajibika kuzungumzia suala
la mchakato wa katiba hasa kutokana na hali tete iliyopo katika Bunge
Maalum la Katiba kufuatia wajumbe wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi
(Ukawa) kususia Bunge Maalum la Katiba.
“Anakwepa
kuzungumzia suala hilo mbele ya vyombo vya habari wakati ndani ya chama
chake anakuwa wa kwanza kushawishi viongozi wenzake wakatae mapendekezo
ya Rasimu ya Katiba yaliyotolewa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba… sijui
kwa nini uwazi unamshinda katika suala hili,” alisema.
Prof.
Baregu alidai vilevile kuwa Mkapa ndiye aliyeshawishi kwamba aliyekuwa
Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba
awasilishe kwanza Rasimu ya Katiba bungeni kabla ya Rais Jakaya Kikwete
kulizindua bunge hilo.
Mhadhiri
wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Benson Bana, alisema Mkapa na
viongozi wengine wastaafu hawawezi kulikwepa suala la mchakato wa katiba
mpya.
Dk.
Bana alisema kwa kuwa Rais Mkapa ni mwanadiplomasia, inawezekana
amesoma alama za nyakati na ndiyo maana anakwepa kuzungumzia suala la
mchakato wa Katiba Mpya.
“Suala
la mchakato wa katiba limekuzwa sana, hata watu wanaokwenda mahakamani
kuhoji wamechelewa, walistahili kufanya hivyo mapema sana na siyo
kusubiri hadi Ukawa (Umoja wa Katiba ya Wananchi) wagome,” alisema.
Kwa
upande wake, Mkuu wa Idara ya Sayansi ya Siasa na Utawala katika Chuo
Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Mohammed Bakari, alisema
kitendo alichokifanya Mkapa kujiweka kando na mchakato wa katiba ni cha
busara kwa kuwa hataki kuonyesha mfungamano na upande wowote.
“Alichokifanya
Mkapa ni cha busara kwani ameitunza heshima yake tofauti na viongozi wa
serikali waliotoa misimamo hivi karibuni, mingi inaegemea ukiangalia
inalenga kukwamisha kupatikana kwa Katiba Mpya,” alisema Prof. Bakari.
Naye
Kaimu Mkurugenzi wa Mtandao wa Jinsia (TGNP), Lilian Liundi, alisema
kitendo cha Mkapa, kujiweka mbali kuzungumzia mchakato wa katiba ni cha
busara.
“Ukiwa
kiongozi ambaye uliwahi kuwa na madaraka makubwa unahitaji kufikiri
mara mbili mbili kabla ya kuzungumza jambo ambalo linaigusa jamii kubwa,
,” alisema Liundi.
TUCTA: MKAPA YUPO SAHIHI
Naye
Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama Vya Wafanyakazi Tanzania (Tucta)
Nicholaus Mgaya, amesena uamuzi wa Mkapa kutoingilia mchakato wa katiba
mpya ni wa busara.
Alisema
Mkapa ametumia busara na kuheshimu mchakato unaoendelea kwani kama
angeongea angekwaza kundi moja wapo kati ya yanayotofautiana katika
mchakato huo.
Alisema
Rais huyo mstaafu ataendelea kuheshimika kutokana na ustaarabu na
busara alizozitumia za kukaa kimya kuzungumzia suala hilo.
LHRC: MKAPA HAWATENDEI HAKI WATANZANIA
KITUO
cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), kimesema ukimya wa Mkapa
kuhusiana mchakato wa Katiba mpya unaoendelea katika Bunge Maalum la
Katiba hawatendei haki Watanzania.
Aidha,
kimesema angetakiwa kutoa maelekezo pale anapoona mambo hayaendi vizuri
kwa bunge hilo kwa kuwa amekuwa rais miaka kumi na anafahamu mambo
mengi.
Mkurugenzi
wa kituo hicho, Dk. Hellen-Kijo Bisimba, alisema busara za Mkapa
zinahitajika katika kushauri juu ya mchakato huo na kutoa maelekezo bila
kumuogopa kiongozi yeyote
“Mkapa
akikaa kimya katika suala hili hawatendei haki Watanzania, busara za
wazee kama yeye zinahitajika kwa kutoa ushauri bila kumuogopa kiongozi
yeyote,” alisema.
Alisema
akiendelea kukaa kimya watu watafikiri kuwa anaogopa kutoa ushauri kwa
kuwa ataliudhi kundi la viongozi fulani wakati jamii inamwamini kwa kuwa
kiongozi anayependa uwazi.
Naye
Mhadhiri wa Chuo Kikuu Cha Ushirika Moshi (MUCCoBS), Dk. Tadey
Msumanje, alisema hatua ya Mkapa kukaa kimya ni jambo la busara kwa kuwa
wao ndiyo watakuwa wasemaji wa mwisho mambo kunasua mchakato
utakapokwama.
Mbunge
wa Bunge la Afrika Mashariki, Shyrose Bhanji, alisema Mkapa kuzungumzia
chochote kuhusu bunge hilo kungesaidia sana kunusuru mchakato huo.
Alisema
viongozi kama hao wanapozungumza neno kuhusu taifa, huwa lina nguvu
zaidi na kwa namna moja ama nyingine linaweza mawazo yao huchukuliwa
kama ushauri.
“Rais
Mkapa alikuwa katika nafasi nzuri ya kusaidia mchakato huu wa Katiba,
hata angetegemewa hata kulitaka liahirishwe kwa sasa mpaka pale
kutakapopatikana mwafaka wa kundi jingine ambalo limetoka katika bunge
hilo,” alisema na kuongeza:
“Bunge
hilo siyo sahihi kuendelea wakati wengine hawapo, japokuwa ni wachache,
lakini kwa sababu ni vema na wao wakasikilizwa na viongozi wakuu kama
hao ndiyo wanaweza kutoa ushauri wa kunusuru mambo makubwa kama hayo.”
WABUNGE WAZUNGUMZA
Mbunge
wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi), David Kafulila, alisema kuwa ukimya
huo wa Mkapa unaashiria kwamba anakwepa majukumu yake kama kiongozi wa
mstaafu wa taifa anayeheshimika na mataifa mengi duniani kutokana na
umahiri wake katika masuala ya kidiplomasia na usuluhishi.
Alisema
huenda Mkapa msimamo wake ni ule ule ambao Kamati Kuu ya CCM imeutoa
wiki iliyopita na kwamba ndiyo maana hataki kuzungumzia hilo kutokana na
kuunga mkono msimamo wa chama chake.
Mbunge wa Rombo (Chadema), Joseph Selasini, alisema Mkapa kukaa kimya
kuzungumzia mchakato wa katiba ni dalili ya kutokuwa na dhamira ya
kutaka kusaidia kulikwamua taifa katika mgogoro ambao unatishia
matumaini ya kupatikana kwa katiba yenye maridhiano.
“Mkwamo
uliopo sasa unaweza ukaondolewa kwa busara ambazo zinatokana na uwapo
wa marais wastaafu akiwamo Benjamin Mkapa ambaye bila shaka anaogopa
kukemea na kushauri kama Watanzania wengine wanavyopendekeza kwa sababu
tu ataonekana mbaya na chama chake,” alisema Selasini.
Mjumbe
wa Bunge Maalum la Katiba kutoka kundi la 201, ambaye hakutaka kutajwa
jina lake litajwe, alisema Rais mstaafu amekataa kuzungumzia mwenendo wa
bunge hilo kwa kuwa atachafuka kisiasa na kumshushia heshima yake mbele
ya Watanzania.
Katibu
wa Chipukizi na Uhamasishaji wa Jumuiya ya Vijana ya CCM (UVCCM), Paul
Makonda, alisema ni sahihi kwa Mkapa kukaa kimya kwa kuwa nia na
matarajio ya Taifa yanajulikana lakini kwa hali ya kubezana.
Alisema heri akae kimya kwa kuwa ukimya nao ni jibu tosha.
TANGA WASEMA MKAPA YUPO SAHIHI
Kwa
upande wa baadhi ya wananchi wa Jiji la Tanga walisema Mkapa kujiweka
kando na mchakato wa Katiba mpya na Bunge Maalum la katiba ni uamuzi wa
busara kwani mwenye mamlaka pekee juu ya suala hilo ni Rais Jakaya
Kikwete.
“Mkapa
ametumia busara kwa sababu sasa hivi kauli moja unayoitoa kila mtu
anaitafsiri kivyake ukisema Bunge liendelee unaonekana wewe ni wa kundi
hili ukisema livunjwe pia utaonekana ni wa kundi jingine,” alisema Onesmo Raymond.
Raymond
ambaye ni mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Cambridge, alisema mwenendo wa
Bunge Maalum la Katiba umechangia kwa kiasi kikubwa kudhoofisha baadhi
ya vyama vya siasa.
Naye
Rose John Mwanaharakati wa masuala ya Maendeleo alisema huenda Mkapa
alishatoa ushauri ambao haukufanyiwa kazi hivyo hana budi kukaa kimya na
kuangalia Taifa linavyokwenda.
Omary
Sekwao, alisema kuwa macho na masikio ya Watanzania kwa sasa
yameelekezwa kwa Rais Kikwete ili kuhakikisha bunge hilo linaleta katiba
iliyo bora na siyo bora katiba.
Jumamosi
iliyopita wakati wa hafla ya chakula cha jioni ya harambee ya Taasisi
ya Benjamin William Mkapa Hiv/Aids (BMAF), mradi wa Mkapa Fellows,
jijini Mwanza, Mkapa alikataa kuzungumzia suala la mchakato wa Katiba.
“Sitaki kuzungumzia suala la Katiba Mpya wala mchakato wake unavyoenda,” alisema kwa kifupi Mkapa.
CHANZO: NIPASHE
0 comments:
Post a Comment