TATA umeendelea kugubika tukio la mtoto kukutwa kwenye boksi katika mtaa wa Azimio mjini Morogoro akiwa ameishi humo kwa miaka mitatu, ambapo sasa imebainika kuwepo kwa shimo lililojaa maji jirani na alipokuwa amefungiwa mtoto huyo.
Shimo hilo kubwa limekutwa chumbani kwa mama mlezi wa mtoto huyo, Mariam Said, hatua chache na mahala lilipokuwa boksi ambalo alikuwa akiishi mtoto huyo mwenye umri wa miaka minne.
Akisimulia mazingira ya kubainika kwa shimo hilo, Mwenyekiti wa Mtaa wa Azimio, Tatu Mgagala alisema Mei 22, polisi walifika kwenye nyumba hiyo wakiwa na mtuhumiwa na kukuta mlango ukiwa umefungwa na waliamua kuvunja ili kuingia ndani kuangalia mazingira ya nyumba hiyo.
Alisema baada ya kuingia ndani ya chumba cha Mariam walikuta kuna giza kutokana na chumba hicho kuzibwa na maboksi na hivyo waliamua kutoa maboksi hayo na ndipo walipobaini kuwepo kwa shimo kubwa lililojaa maji jirani na boksi alimokuwa amehifadhiwa mtoto huyo, huku eneo hilo likiwa ndilo pekee likiwa halijasakafiwa saruji.
Mgagala alisema baada ya polisi kuliona shimo hilo, walimuuliza Mariam sababu ya uwepo wa shimo hilo lenye maji huku akijua kuwa kuna ugonjwa wa homa ya dengue ambapo alidai maji hayo huyatumia kunawa miguu na mikono usiku kabla ya kulala.
Hata hivyo, pamoja na Mariam kudai kuyatumia maji hayo kunawa miguu na mikono kila siku usiku kabla ya kulala, ilibainika Polisi kuwa yeye na mumewe kwa muda mrefu walikuwa hawajaoga na hivyo kulazimishwa kuoga wakiwa mbaroni.
Katika hatua nyingine, mtetezi wa haki za watoto, Peter Mwita alisema watuhumiwa Mariam, mumewe Mtonga Omari na baba mzazi wa mtoto huyo, Rashid Mvungi, watafikishwa mahakamani leo kujibu mashitaka yanayowakabili.
Akielezea hali ya afya ya mtoto, Mwita alisema hadi sasa tayari amepimwa vipimo vyote kikiwemo kipimo cha damu kubwa na hajabainika kuwa na virusi vya Ukimwi zaidi ya homa ya mapafu (nimonia) na matatizo ya mifupa.
Alisema ili kuhakikisha matunzo ya mtoto huyo yanakuwa mazuri, wamemtafuta mama wa kumlea mtoto huyo ambaye atakuwa analipwa kwa kazi hiyo.
Mama huyo Josephina Joel akizungumzia majukumu aliyokabidhiwa, alisema amechukuliwa kutoka katika kambi ya kulea wazee ya Fungafunga ya mjini hapa na kuongeza kuwa anajua uchungu wa watoto, hivyo kwake anaona hakuna changamoto zozote anazopata kwa kumlea mtoto huyo.
Alisema mtoto huyo hupendelea kula chipsi mayai, wali nyama au samaki pamoja na juisi, lakini hukataa kula ugali na maziwa.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
0 comments:
Post a Comment