Kwako mheshimiwa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo.
Najua hunifahamu na hakuna mazingira yanayoweza kunikutanisha na wewe na ndiyo maana nimeamua kutumia ukurasa huu kufikisha ujumbe wangu kwako, ambao najua hutaufurahia.
Mheshimiwa, mimi sikuzaliwa Juni 25, 1954 huko Musoma kama wewe. Mimi si msomi mwenye ‘CV’ ya nguvu na kubobea kwenye sayansi ya miamba na madini kama wewe. Sijawahi kufundisha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam wala sijawahi kujiunga na chama au taasisi yoyote ya kisayansi duniani kama wewe.
 
 
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo.
Sijawahi kufanya kazi kama mtafiti kwenye Chuo Kikuu cha Mainz, Ujerumani kama wewe wala mimi sijawahi kuteuliwa kuwania ukurugenzi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (Unesco). Mimi si mbunge wa kuteuliwa wala waziri mwenye dhamana kubwa kama wewe.
Mimi ni kilaza tu, nisiyekuwa na elimu yoyote kichwani, niponipo tu mjini naganga njaa kuhakikisha mkono unaenda kinywani.Hata hivyo, pamoja na ukilaza wangu, ningekuwa mimi katika nafasi yako, kwa hii kashfa kubwa ya mabilioni ya fedha yaliyochotwa kwenye akaunti ya Tegeta Escrow inayoendelea kuitafuna nchi, nakuapia kuwa tayari ningeshang’atuka madarakani.
Nisingesubiri sijui ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Serikali (CAG), uamuzi wa bunge wala mahakama, dhamira yangu ingenisuta kwamba madudu haya yamefanyika kwenye wizara yangu kwa kuhusisha Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Ningeona aibu kwamba dhamana kubwa niliyopewa na mheshimiwa Rais Jakaya Kikwete kwa niaba ya Watanzania, ya kuhakikisha rasilimali zao zinawanufaisha wazawa, imenishinda.
Nasikiasikia kwamba eti na wewe ni miongoni mwa vibosile waliochota zile shilingi bilioni 306 na kuzitia mfukoni, sina uhakika wala siwezi kuthibitisha hilo kwa kuwa mimi siyo mahakama lakini ile kutajwatajwa tu, hata kama si kweli, kungetosha kukufanya uachie madaraka na kupisha uchunguzi.
Ndiyo! Unawezaje kuingia ofisini kwa kujiamini na mwisho wa mwezi ukaenda kukinga mshahara mnono wakati kazi uliyopewa imekushinda? Mahakama ilipoamuru kwamba fedha (service charge) zilizokuwa zinalipwa na Tanesco kwa IPTL, zipelekwe kwenye akaunti maalum, Tegeta Escrow mpaka muafaka utakapofikiwa kati ya wabia waliokuwa wanahusika katika kesi hiyo, ilikuwa na lengo zuri la kunusuru fedha za umma.
Sasa iweje hata hukumu bado haijatolewa, watu ‘wajisevie’ mabilioni ya fedha chini ya wizara yako na BoT, huku wewe uliyepewa dhamana ya juu kabisa katika wizara, ukilifumbia macho suala hili?
Najua wewe ni msomi ambaye elimu yako imekukomboa ipasavyo. Naamini kwamba wewe si mwanasiasa bali mtendaji ndiyo maana mheshimiwa rais alikupa nafasi hiyo nzito ili kuwatumikia Watanzania lakini mbona mambo yamekuwa ndivyo sivyo?
Nilisikia kauli yako uliyoitoa wakati ukihutubia kwenye mkutano wa wawekezaji zaidi ya 170 kutoka nchi mbalimbali duniani hivi karibuni kujadili kuhusu mbinu za kulipatia Bara la Afrika umeme wa uhakika.
Ukasikika ukisema eti fedha zilizokuwa katika akaunti ya Tegeta Escrow siyo za umma bali ni za Kampuni ya IPTL na ukawataka ‘akina yakhe’ kuacha kuzikomalia kwani siyo zao, ukadiriki kuwaita majina mabaya wote wanaolishupalia suala hilo na kutaka wapuuzwe.
Sawa, uelewa wako ni mkubwa na unajua mambo mengi zaidi makubwa lakini kama kweli wewe ni muungwana, kubali kuwajibika kwanza. Acha kuleta siasa mheshimiwa, ndugu zetu wanakufa Muhimbili kwa kukosa dawa wakati mabilioni yamechotwa chini ya wizara yako.
Nguo ikimvuka, muungwana huchutama. Ningekuwa mimi katika nafasi yako, tayari ningeshang’atuka ili kulinda heshima yangu, kupisha uchunguzi na kuwaachia wenye uchungu na nchi hii walinde rasilimali zetu.
Wasalaam. TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
LIKE PAGE YETU HAPO PIA SHARE STORY NA RAFIKI ZAKO

0 comments:

Post a Comment

BURUDANI

 
Top