Kungu Masanja akiwa ndani ya gari la polisi

Wakazi wa kijiji cha Chibe kata ya Chibe katika manispaa ya Shinyanga wamepigwa butwaa baada ya mjumbe wa serikali ya kijiji hicho Kungu Masanja kukamatwa na askari polisi akiwa ameshikilia bango katika mbio za Mwenge wa Uhuru katika kijiji cha Chibe.

Kungu Masanja ambaye pia ni katibu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) katika kijiji cha Chibe alikutwa amebeba bango wakati kiongozi wa mbio za mwenge wa Uhuru mwaka huu Rachel Stephen Kassanda akifungua zahanati ya kijiji hicho.

Baadhi ya maneno yaliyokuwa yanasomeka katika bango hilo ni “KIONGOZI WA MBIO ZA MWENGE KITAIFA. 
I. HIVI MAPATO NA MATUMIZI YA ZAHANATI YA KIJIJI HUSOMWA WAPI?
II. HUJUI JENGO LA DAKTARI HARINA KIWANGO, KAMA HUJUI PITA NDANI YAKE.
III. KWA HOYO MACHACHE NITALALA TU POLISI.”

Muda mfupi baada ya kuonekana na bango hilo ghafla askari wa jeshi la polisi mkoa wa Shinyanga walimkamata na kuondoka naye huku wakazi wa eneo hilo wakibaki midomo wazi.

Akizungumza akiwa chini ya ulinzi wa askari polisi Masanja alidai kuwa aliyoyaandika yako sahihi na kwamba hajashawishiwa na mtu yeyote ameamua kuandika ujumbe ili ufanyiwe kazi.

Akizungumza na Malunde1 blog diwani wa kata hiyo Mahona Gwisu Kameja kupitia Chama Cha Mapinduzi alisema alishangaa kumwona kijana huyo akiwa ndani ya gari la polisi.

“Binafsi sikuona bango hilo, wala sikumwona wakati anakamatwa, hilo jengo analodai liko chini ya kiwango lilijengwa mwaka 2009 kwa nguvu ya wananchi, serikali na TASAF likigharimu shilingi milioni 52 Tangu mwezi Septemba 2014 linatumiwa na mganga na wauguzi wa zahanati iliyozinduliwa leo,” alisema Diwani huyo.

“Hata hivyo mimi nashangaa huyu kijana ni mjumbe wa serikali ya kijiji. Kama limejengwa chini ya kiwango basi yeye anapaswa kuwajibika, haiwezekani mjumbe wa kijiji ajikaange mwenyewe. Hapa kuna UCHADEMA maana huyu ni kiongozi wa CHADEMA katika kijiji hiki. Labda katumwa,” aliongeza diwani Kameja.

Naye mkurugenzi wa manispaa ya Shinyanga Festo Kang’ombe aliiambia Malunde1 blog kuwa jengo hilo limejengwa katika kiwango kinachotakiwa ndiyo maana linatumika hivi sasa.

Kwa upande wake kiongozi wa mbio za mwenge wa uhuru 2014 Rachel Stephen Kassanda alisema jengo lililotengenezewa bango siyo lile la zahanati waliyoifungua hivyo hawezi kulizungumzia.

Kassanda alisema mamlaka/majukumu aliyopewa katika mbio za mwenge ni kuzungumzia miradi iliyoko kwenye ratiba aliyopangiwa hivyo suala hilo wanaohusika ni halmashauri husika.

Kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga Justus Kamugisha alipotafutwa na mwandishi wa habari hizi kuzungumzia kuhusu kukamatwa kwa kijana huyo alisema yuko nje ya ofisi, ingawa hata kaimu kamanda wa polisi Longinus Tibishishubwa alipopigiwa simu zaidi ya mara moja haikupokelewa siku hiyo.
Kungu Masanja akiwa ndani ya gari la polisi muda mfupi baada ya kuonekana na bango kwenye mbio za Mwenge wa Uhuru kaitka Kata ya Chibe, Manispaa ya Shinyanga

Malunde1 blog: ANGALIA PICHA_KIONGOZI WA CHADEMA AKAMATWA AKIWA NA BANGO KWENYE MWENGE WA UHUR TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
LIKE PAGE YETU HAPO PIA SHARE STORY NA RAFIKI ZAKO

0 comments:

Post a Comment

BURUDANI

 
Top