Dar
es Salaam. Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi amesema
Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) unakabiliwa na changamoto kubwa
suala la ruzuku.
Ingawa hakutaka kuingia kwa undani kuelezea changamoto hiyo, Jaji
Mutungi alisema anaona ugumu wa Ukawa katika kushughulikia tatizo hilo,
lakini akaongeza kuwa wakati ukifika ofisi yake italizungumza.
Alisema hayo jana alipotakiwa kutoa maoni yake kuhusu uamuzi wa vyama
hivyo vinne kuamua kushirikiana katika chaguzi zijazo na tafsiri yake
kisheria.
Jumapili Chadema, NCCR-Mageuzi, NLD na CUF vilisaini makubaliano ya
kushirikiana katika mambo saba, likiwamo la kusimamisha mgombea mmoja
katika ngazi zote kuanzia chaguzi za serikali za mitaa hadi Uchaguzi
Mkuu ujao.
Jaji Mutungi alisema: “Maswali hayo unapaswa kuwauliza wao. Tutakuja
kuzungumza wakati ukifika. Suala la ruzuku lina taratibu zake, Muungano
una taratibu zake na ushirikiano pia,” alisema.
“Ruzuku ni changamoto katika suala la Ukawa, lakini sitaki kuingilia hilo kwa kuwa ukifika wakati tutasema.”
Alisema kwa sasa nchi inaelekea katika uchaguzi, hivyo ni muhimu kwa
Ofisi ya Msajili ikaacha kuingilia hayo. “Lazima niwe careful (makini)
katika mazungumzo yangu, kwani naweza nikawa mimi na wewe (mwandishi)
tunatafsiri sheria, lakini wengine wakafikiria kisiasa,” alisema Jaji
Mutungi.
Kifungu cha 18 cha Sheria ya Vyama vya Siasa ya Mwaka 2002 kinaeleza
kuwa ruzuku ambazo chama kitapewa zitakuwa ni kwa ajili ya shughuli za
chama husika bungeni, shughuli za kijamii za chama husika, suala lolote
la uchaguzi ambalo chama kimeteua mgombea na kitu chochote muhimu
ambacho chama kitakuwa kinafanya.
Kifungu hicho kinaeleza kuwa ruzuku ambazo chama kinapata lazima zikaguliwe na kuwasilishwa hesabu kwa Msajili wa Vyama.
Changamoto hiyo inatokana na ukweli kwamba kuunganisha nguvu
kutamaanisha kuwa chama kitakubaliwa na Ukawa kusimamisha mgombea urais,
ndicho kitakachonufaika na ruzuku, ambayo kwa kiasi kikubwa hutokana na
uwingi wa kura anazopata mgombea wa nafasi hiyo.
Chadema, ambayo mgombea wake wa urais katika uchaguzi uliopita, Dk
Wilbroard Slaa alipata kura 2,271,941, kinapata ruzuku ya Sh203.6
milioni kwa mwezi, wakati CUF inapata ruzuku ya Sh117.4 milioni baada ya
Profesa Ibrahim Lipumba kupata kura 695,667.
NCCR-Mageuzi inapata ruzuku ya Sh10 milioni wakati NLD haipati ruzuku yoyote kutokana na kutokuwa na wabunge.
0 comments:
Post a Comment