Matukio ya mauaji ya watu wasio na hatia, yameendelea kuuandama Mkoa wa Geita, kufuatia watu watatu kuuawa kwa kukatwa mapanga na kuchomwa mkuki huku mmoja akijeruhiwa baada ya mtu mmoja anayesadikiwa ni mgonjwa wa akili kutekeleza unyama wake. 
Tukio hilo lililotokea jana asubuhi katika kijiji cha Nyamilyango wilayani Geita, na aliyejeruhiwa na kulazwa katika Hospitali ya Wilaya ya Geita ni Mathayo Sindamsanga, na hali yake imeelezwa ni mbaya. Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo, Dk. Adam Sijaona, alithitibisha kupokea miili mitatu iliyohifadhiwa hospitalini hapo pamoja na majeruhi mmoja.

Dk. Sijaona aliwataja waliouawa kuwa ni Pindo Makono, Ndakazi Bertha Masabile na Jacob Bukulu, ambao ni wakazi wa kijiji hicho.

Hata hivyo, mtu huyo aliyesababisha mauaji hayo, alikamatwa na wananchi wenye hasira na kisha kumfikisha kituo cha polisi.

Dk. Sijaona alisema marehemu hao walifariki dunia kutokana na kuvuja damu nyingi mwilini kufuatia muuaji kutumia panga na kuwacharanga na kisha mkuki kuwatoboa miili.

Akizungumzia tukio hilo, Diwani wa Kata ya Bugulula, Elisha Lupuga, alisema lililotokea juzi saa 1:00 jioni katika kitongoji cha Misheni katika kijiji cha Nyamilyango baada ya mtuhumiwa, Rashid Ramadhani, mkazi wa kijiji hicho kutumia mkuki na panga kuwaua watu hao.

“Dhamira yake mpaka sasa haijafahamika ilikuwa nini, lakini amekuwa na tabia ya kuvuta bangi kwa muda mrefu, hivyo tunahisi amevurugukiwa akili yake,” alisema Lupuga.

Hata hivyo, Lupuga alisema baadhi ya waliouawa walikuwa na mahusiano na mtuhumiwa, lakini hakufafanua ni mahusiano ya namna gani waliyokuwa nayo.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Geita, Joseph Konyo, alithibitisha kutokea tukio hilo na kwamba mtuhumiwa anashikiliwa katika kituo cha polisi akisubiri hatua za kisheria kuchukuliwa dhidi yake.

Tukio hilo limeibua upya simanzi na vilio kwa wananchi wa mkoa huo ambao mara kwa mara wamekuwa wakikumbwa na matukio ya mauaji ya aina mbalimbali.

Hilo ni tukio la pili ndani ya wiki moja baada ya usiku wa kuamkia Septemba 7, mwakahuu, watoto wanne wa familia moja kuuawa kufuatia nyumba yao kuteketezwa na moto katika kitongoji cha Elimu kata ya Kiangalala wilayani Geita.

Watoto walioteketea na moto huo ni Reginald Robert (9) mwanafunzi wa darasa la nne na Sofia (6) wa Shule ya Msingi Ukombozi na Remijius (4) wa chekechea pamoja na Scolastika (15) aliyekuwa akisoma shule ya sekondari Mwatulole.
 
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
LIKE PAGE YETU HAPO PIA SHARE STORY NA RAFIKI ZAKO

0 comments:

Post a Comment

BURUDANI

 
Top