Baadhi ya wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba wamesema wala rushwa pamoja na wahujumu uchumi adhabu yao iwe ni kunyongwa.
Wametaka Katiba mpya inayoenda kuandikwa itamke hivyo ili kufanya viongozi wa kisiasa kuogopa kama ilivyo kwenye nchi nyingine.
Sababu ya wajumbe hao kupendekeza jambo hilo ni kwamba uhujumu uchumi na rushwa nchini limekuwa tatizo kubwa kwa viongozi.
Kutokana na ukiukwaji huo wa maadili, wamesema umefika wakati wa kuweka bayana suala hilo kwenye sheria mama.
Miongoni
mwa waliochangia ni Paul Makonda aliyesema suala hilo likiwekwa
bayana, litaokoa fedha nyingi za walipa kodi ambazo kwa sasa baadhi ya
viongozi wanazichota na kwenda kuzihifadhi nje ya nchi.
Pia alipinga kuruhusu viongozi wa nchi kufungua akaunti nje ya nchi. “Kwa nini viongozi hao washindwe kuhifadhi fedha zao ndani ya nchi, wanafanya biashara gani hadi wakafungue benki nje ya nchi?
“Tusiruhusu jambo hili na napendekeza kwamba kiongozi atakayebainika amekula rushwa na kuhujumu uchumi huyo anyongwe,” alisema Makonda.
Yusuf
Singo pia alisema maadili yanazidi kuporomoka kwa viongozi, jambo
linalorudisha nchi nyuma. Alitaka Katiba isisitize maadili kwa kada hiyo
na ambao watakiuka wanyongwe.
Alitoa
mfano wa Japan kuwa kiongozi wa kisiasa anapochunguzwa kwa kujihusisha
na rushwa anatoa machozi kwa sababu hajui hatima yake. “Tunataka na sisi ifike wakati kiongozi akianza kuchunguzwa atoe machozi,” alisema.
Dk
Mary Mwanjelwa katika mchango wake alisema rushwa imekuwa adui mkubwa
wa maendeleo ya Watanzania. Alisema isipopingwa kuanzia kwenye Katiba,
nchi itakuwa inajichora.
Alisema
Bunge halitaeleweka kama halitaweka jambo hilo kwenye Katiba, kwa
sababu wananchi wengi wameteseka ndani ya nchi yao kwa sababu ya rushwa.
Alisema pia wapo viongozi wengi wasio na maadili na ndiyo maana wanajihusisha na vitendo vya rushwa.
Kwa
upande wake, Profesa Mark Mwandosya alisema tatizo la rushwa haliwezi
kutenganishwa na haki za binadamu kutokana na kukosesha wananchi
maendeleo.
Profesa Mwandosya alisema Katiba lazima itambue adui wa haki za wananchi ni rushwa.
Alipendekeza
suala hilo litambulike kikatiba na serikali zote mbili zitunge sheria
kali za kupambana na rushwa kuhakikisha wananchi wanapata haki zao za
msingi bila kutoa wala kupokea rushwa.
Naye Gerison Lwenge alisema Katiba itambue jambo hilo na ikemee vikali kwa wanaotoa na wale wanaopokea.
Alisema kwa ahli ilivyo, wanaobanwa zaidi ni wale ambao wanapokea na akapendekeza sheria kali zitungwe kubana pia wanaotoa.
Alishauri Kamisheni isimamie suala hilo la rushwa badala ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).
Kwa
mujibu wa Lwenge, Kamisheni ni chombo kikubwa zaidi kuliko ilivyo kwa
taasisi. Alisema kazi yake itakuwa ni kuzuia zaidi na si kutibu pekee.
Jesca Msambatavangu alisema Takukuru wanafanya kazi vizuri na walishindwa kupambana na rushwa kwa vile hawana uhuru wa kutosha.
Alisema
kama Takukuru wakipewa meno kupitia Katiba mpya, watashughulika kwa
uhuru zaidi katika kupambana na tatizo la rushwa nchini.
0 comments:
Post a Comment