Mtuhumiwa Geofrey Kilangwa ‘Simbaiwe’( katikati) aliyemuua mwanaye mwenye umri  wa mwaka mmoja na miezi miwili, Regina Geofrey.
 

YULE mtoto wa umri  wa mwaka mmoja na miezi miwili, Regina Geofrey aliyeuawa kikatili kwa kunyongwa kisha kuzikwa na baba yake mzazi, Geofrey Kilangwa ‘Simbaiwe’ (27) kwa kuwa alizaliwa akiwa ametanguliza makalio yake, amezidi kuibua maswali.Baadhi ya wakazi wa Katavi waliozungumza na gazeti hili juzi, walihoji uhalali wa baba kumjadili mtoto katika kuzaliwa kwa sababu ya kutanguliza kiungo fulani.Wengine walitaka kujua ni kwa nini kama kumuua mtoto wake, mzazi huyo alisubiri kwa mwaka mmoja na miezi miwili? Mtuhumiwa ambaye pia ni mganga wa kienyeji anayeishi Kitongoji cha Mwikang’ombe, Kijiji cha Katuma wilayani Mpanda, alitenda unyama huo  kwa madai kuwa mtoto huyo alizaliwa akiwa ametanguliza makalio, hivyo ni nuksi kubwa katika shughuli zake za uganga wa kienyeji, madai yaliyopingwa na watu mbalimbali, zikiwemo taasisi za kutetea haki za binadamu. 



Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi, Dhahiri Kidavashari,  akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa, alidai mzazi  huyo  alitenda uhalifu huo Agosti 20, mwaka huu ambapo alikamatwa na Jeshi la Polisi, Agosti 26. 
Ilidaiwa  siku hiyo ya tukio,  mtuhumiwa huyo  baada ya kumnyonga hadi kufa binti yake, alimzika kwa siri katika  kibanda  chake anachofanyia shughuli za uganga.
Kamanda Kidavashari alisema mtoto Regina alikuwa anasumbuliwa na ugonjwa ambao haukufahamika  kwa zaidi ya mwezi mmoja.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi, Dhahiri Kidavashari.
 “Ndipo  baba mzazi  wa  binti huyo  alipomchukua marehemu na kwenda kumuuguza kwa siri pasipo mama  yake mzazi kufahamu kwani alimdanganya kuwa mtoto wao amepelekwa  kutibiwa na babu yake mkoani Mwanza,” alisema Kidavashari. 

Kwa mujibu wa Kamanda Kidavashari, wakazi  wa kitongoji hicho wakiongozwa na mwenyekiti wao, walimtilia shaka mtuhumiwa kutokana na tetesi zilizosambaa kwamba, Regina aliuawa na baba yake mzazi na kuzikwa kwa siri. 
Mwenyekiti huyo na wakazi wa eneo hilo walifika nyumbani kwa mtuhumiwa na kuhoji alipo binti yake, aliposhindwa kujibu wakasema wampekue ambapo alipinga vikali  lakini alipopekuliwa  kibandani kwake  walibaini kuwepo kwa tuta dogo lililokuwa  limechimbwa siku za karibuni. 
Wakazi hao walifukua tuta hilo  na kukuta kichwa cha mtoto Regina na ndipo wakalitaarifu jeshi la polisi. 
 Mama wa marehemu, Maria Exavery (22) alisema hakupewa taarifa kwamba binti yake  amekufa.
“Mimi nilikuwa nafahamu Regina yuko kwa babu yake Mwanza akitibiwa,” alisema huku akimwaga machozi. 
Naye Regina Kaboni (40), mkazi wa Isamilo Mwanza  ambaye alikuwa akitibiwa na mtuhumiwa,  anadai kuwa alishirikishwa katika maziko ya binti huyo baada ya kufa.“Hata hivyo, nilishtushwa sana kwa kitendo cha mtuhumiwa kumzika  mwanaye  bila mkewe, nilipomuuliza akadai mila za kwao mtoto aliyezaliwa  kwa kutanguliza makalio, mama mzazi  wa mtoto ni mwiko kushirikishwa katika maziko. 
Kwa mujibu wa Kidavashari watu wanne, wakiwemo  wazazi  wa marehemu  wanashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa mahojiano zaidi ambapo watafikishwa mahakamani mara tu  baada ya upelelezi kukamilika.
 Wengine wanaoshikiliwa na jeshi hilo  ni Regina Kaboni na Msolwa Jacob (29), mkazi wa Kitongoji cha Mwikang’ombe.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
LIKE PAGE YETU HAPO PIA SHARE STORY NA RAFIKI ZAKO

0 comments:

Post a Comment

BURUDANI

 
Top