Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willbrod Slaa amemtaka Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Seif Rashid kujiuzulu kutokana na sakata la utupaji viungo vya binadamu katika Bonde la Mto Mpiji, Dar es Salaam. 
Akizungumza katika hafla ya kuuaga uongozi wa Chama cha Wanafunzi wa Vyuo Vikuu wa Chadema (Chaso) na kufungua Tawi la Chuo Kikuu cha Sayansi ya Afya na Tiba Muhimbili (Muhas) jana, Dk Slaa alisema utupaji wa viungo hivyo ni udhalilishaji mkubwa wa binadamu na kwamba Serikali inatakiwa kuwajibika moja kwa moja.
“Inashangaza kuona miguu, mikono, pua vinatupwa dampo na Serikali na viongozi wake bado wamesimama. Halafu unafunga hospitali ili umuathiri nani? Si unawaathiri wanafunzi wa chuo hicho wanaoitumia kujifunza?” alisema na kuongeza:
“Nilitarajia waziri angejiuzulu tangu siku ya kwanza baada ya kubainika vile viungo na asingejiuzulu basi Rais Jakaya Kikwete amfukuze kazi.”
Dk Slaa alisema Serikali imelegalega katika udhibiti wa viungo vya binadamu ambavyo hutumiwa na madaktari kujifunzia kwa kukosa sheria madhubuti ya kudhibiti taratibu za matumizi yake.
“Niambieni kama kuna sheria ya kuharibu miili ya binadamu hapa nchini na hivyo viungo vinavyoingizwa kutoka nchi za nje vinaongozwa na sheria gani? Huwezi  kuwa na madaktari halafu huna sheria,” alisema Dk Slaa.
Mapema wiki iliyopita viliokotwa viungo vya binadamu katika bonde hilo vikiwa katika mifuko myeusi na baadaye vilibainika kuwa vilitoka katika Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Tiba na Teknolojia (IMTU).
Tayari viongozi wanane wa chuo hicho wamekamatwa na Polisi na Serikali imeunda timu ya wataalamu kuchunguza na mwishoni wa wiki iliifungia Hospitali ya IMTU kwa kukosa sifa ya kutoa huduma za matibabu.
Akisoma risala kwa niaba ya uongozi wa Chaso-Muhas unaomaliza muda wake, mwenyekiti mstaafu wa tawi hilo, Elias Mwakapimba alisema wanakabiliwa na changamoto za uhaba wa vifaa vya kusomea, upendeleo wa ajira na kuzuiwa kufanya siasa chuoni.
slaa
Dk. Slaa

Pia, wanafunzi hao waliiomba Serikali iongeze bajeti katika sekta ya afya ili iliweze kuzalisha wataalamu wengi na kuwapa motisha ya kufanya kazi kwa ufanisi.
Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Mashariki na Pwani, Profesa Abdallah Safari aliwataka wanafunzi hao kusimamia harakati za mapinduzi ya kisiasa na kuwataka wasiogope vitisho vinavyotolewa na CCM.
“Kazi ya wasomi ni kujitoa muhanga ili kuwakomboa wanyonge wengi… lazima msimame imara msiyumbishwe na mabwanyenye wanaotaka kuyumbisha harakati zenu,” alisema Profesa Safari
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
LIKE PAGE YETU HAPO PIA SHARE STORY NA RAFIKI ZAKO

0 comments:

Post a Comment

BURUDANI

 
Top